Takriban katika maisha ya
wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti.
Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na
uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake kama tulivyoona katika
makala iliyopita ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa
hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.
Hivyo basi, sababu kubwa ya
wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo
atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa
yao, na katika makala yetu ya mwanzo tulianza kuangalia baadhi ya visababishi
vinavyopelekea katika kuchokana kwa wanandoa.
Leo InshaAllaah tutaendelea
kuangalia na kuchambua visababishi vengine ambavyo ni muhimu kwa wanandoa
kuvielewa, hususan mwanamke.
d- Kutamka na kudhihirisha mapenzi: Ni muhimu sana kwa wanandoa ili kuyaimarisha
mapenzi yao yasiote mvi, kutamkiana hisia zao za kupendana bila utangulizi
wowote, kwa mume au mke kumwambia mwenzake NAKUPENDA kuna athari nzuri katika
nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama. Na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
ametufundisha haya kwa kusema:
(Atakapompenda
mmoja wenu ndugu yake basi amfahamishe, kwani huzidisha maelewano na
kuthibitisha mapenzi) Hadiyth Sahihi,
Silsilatus Swahiyhah
Haya ni
mafundisho ya Kiislamu ambayo leo hii yanaonekana ni mila za kimagharibi, na
huonekana kioja katika jamii mke kumwambia mumewe kuwa ‘Nakupenda’ na si ajabu
mume mwenyewe au mke anayeambiwa hivyo na mwenzake akajibu kwa hayaa “ Ah hebu
acha utani wako, sisi tumeishazeeka”. Lakini wanandoa wengi hupenda
kudhihirisha mabaya na mambo yanayowakera kuliko yale mazuri ya kufurahisha, jambo
ambalo kwa kiwango kikubwa linachangia katika kuchokana haraka.
e- Kupeana zawadi: Zawadi ni njia
nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako na
nafasi ya mwenzako katika maisha yako, na zawadi ambayo
mtu huitoa kwa mwenzake bila ya utangulizi au mnasaba maalum huleta athari
njema na huimarisha mapenzi, kama tulivyofundishwa na Mtume wetu (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth
aliyosimulia Abu Hurayrah:(Peaneni zawadi mtapendana)
Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy
Na katika
zoezi hili la kupeana zawadi, ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda
mwengine ili zawadi iwe na athari inayotarajiwa, na iwe ni zawadi maalum kwa
mlengwa, isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo, kwa mfano,
si vema kwa mwanamme kumletea mkewe zawadi ya sufuria, microwave, pazia, Dinner
set, hiyo haitaitwa zawadi, lakini ni juu yake kumletea manukato ayapandayo,
hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu, na vitu ambavyo ni maalumu kwa
matumizi yake binafsi. Hali kadhalika kwa mwanamke kumzawadia mumewe achunge
vigezo hivyo.
f- Kualikana vyakula:
Inaweza kushangaza kuwa vipi wanandoa wataalikana chakula wakati wenyewe ni
mume na mke, na ni lazima wale pamoja?! Ni vema ikaeleweka kuwa, kubadili
mazingira na kufanya vitu makhsusi kwa kushtukizana, huwafanya wanandoa
kutozoeana na kuchokana, kwani maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja
kila siku humfanya mtu kuyachoka, ni vema wanandoa na hasa mwanamke kuwa
mbunifu katika kuyapaka rangi mpya maisha yao kwa kubuni vitu vitakavyo tia
ladha mpya katika nyumba, njia mojawapo ni hiyo ya kumualika chakula
maalum mumewe peke yake, na hata kama itamlazimu kununua au kuagiza aina
tofauti ya chakula basi afanye hivyo, na ampe mwaliko mumewe wa kutokosa
kuhudhuria katika mnasaba huo. Aidha mwanamume naye anaweza kumualika mkewe
katika hoteli ya heshima mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya
kujikumbusha mambo mazuri yaliopita.
g- Kubadilisha mpangilio wa nyumba:
Wanawake wengi huwalalamikia waume zao kwa kutopenda kukaa nyumbani na badala
yake kumaliza muda wao kwenye migahawa na kwa marafiki zao. Mke mwerevu huwa
anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi
yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba, kwani mazingira ya nyumba
yanapokuwa ni yale yale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu,
kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka
imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa basi rangi ni
zilezile, hali hii humfukuza mwanamume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala
tu, na huu ndio mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba.
h- Usafi wa mwili na mavazi:Moja
miongoni mwa mambo yanayokera kwa wanandoa ni uchafu wa mmoja wao, uchafu ni
sifa isiyovumilika hususan kwa mwanamke, baadhi ya wanawake hudhani kuwa manukato,
vipodozi ndio usafi, utakuta anapitisha masiku bila kuoga kikamilifu, bali
anapitisha pitisha maji na sabuni tu katika maeneo fulani, kisha kujijaza
manukato, lotion na mafuta mengine, bila kuelewa kuwa, anapokuwa karibu zaidi
na mumewe harufu ya asili hujitokeza na kuleta mchanganyiko wa harufu mbaya,
hali kama hii si rahisi kwa mwanaume mstaarabu kuizungumzia kwa mkewe, atakaa
nayo na atavumilia, lakini mwisho wake ni kumchoka mke huyu. Wanaume nao
hudhani kuwa kwao wanaume ndio wamepewa kibali cha kuwa wachafu, kwa mfano
wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho, na wengine wana matatizo
sugu ya kunuka miguu, huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi, aidha
baadhi ya wanaume hawana vionjo katika mavazi yao, na jinsi wanavyojiweka, jambo
ambalo linaweza kumsababishia mke maudhi, na hata kujihisi aibu kunasibishwa na
mume wake.
i- Kufanya Ibada za Sunnah
kwa pamoja: Nguzo muhimu na mhimili wa maisha
ya ndoa ni kumcha Allaah, Swalah za usiku humkurubisha mja karibu zaidi
na Allaah, hivyo mume na mke kuhimizana kufanya ibada hii pamoja
huwazidishia imani na mapenzi baina yao na kuifanya ndoa yao kuwa imara zaidi,
aidha hata funga za Sunnah za Jumatatu na Alkhamiys ni vema mume na mke
wakazifunga pamoja kama hali itaruhusu hivyo. Na ni vema wakaweka katika
kalenda yao ya mwezi au miezi kwa mujibu wa nafasi zao, kutembelea Ndugu
wa nasaba, kutembelea Majirani, kutembelea wagonjwa Hospitali, kutembelea Vituo
vya Watoto Yatima, kujitolea katika Taasisi za Kiislamu kwa kufanya kazi au
kutoa ujuzi walionao. Ibada hizi zitawazidishia imani yao na kuwafanya wawe
karibu na Allaah na wawe karibu na ndoa yao.
Imeandikwa na; Shams
Elmi (Abu ‘Ilm)
Chanzo Al hidaya

No comments:
Post a Comment