Dec 23, 2013

NIYONZIMA WA YANGA BADO HAAMINI KABISA!


HADI mwamuzi Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Zanzibar anapuliza filimbi ya kumaliza mchezo, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima hakuamini kama timu yake imepigwa mabao 3-1 dhidi ya Simba juzi Jumamosi.
Niyonzima raia wa Rwanda alicheza kama winga katika mchezo huo wa kirafiki uliopewa jina la Nani Mtani Jembe huku akiwa mmoja wa wachezaji wa Yanga waliocheza kwa dakika 90.
Akizungumza na Mwanaspoti, Niyonzima alisema haamini kama mchezo huo umeisha wakiwa wamefungwa mabao 3-1, kwani walikuwa na kila kitu cha kuwawezesha kushinda.
“Sijui nikuambiaje, sijui nini kimetukuta maana tulikuwa na kila kitu uwanjani. Unajua hii ni mechi kubwa na hata kabla ya mechi hii nilikuambia hakuna mechi ya Simba na Yanga ambayo ni ndogo.
“Wenzetu wamecheza kwa kutumia nafasi walizopata kwa manufaa, sisi tulijitahidi lakini ndiyo kama ulivyoona mambo yalikuwa hayakamiliki, hivi ni vitu vinavyoweza kutokea muda wowote wa mchezo,” alisema Niyonzima ambaye alipiga krosi iliyozaa bao dakika ya 87.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Amisi Tambwe aliyefunga mawili na Awadh Juma aliyefunga moja huku lile la Yanga likifungwa na Emmanuel Okwi.





No comments:

Post a Comment