Dec 23, 2013

TAMBWE AMFUNIKA OKWI, YANGA MAJANGA MATUPU

Dar es Salaam. Mshambuliaji Amis Tambwe ameitibua sherehe ya utambulisho wa Emmanuel Okwi baada ya kupachika  mabao mawili wakati Simba ilipoichakaza Yanga 3-1 katika mchezo wa ‘Nani Mtani Jembe’ jana kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam.
Mrundi Tambwe  alifunga mabao mawili huku Awadh Juma akifunga bao moja kwa Simba kabla ya Okwi kufunga bao la kufutia machozi kwa Yanga.
 


Tambwe aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 13 baada ya kupokea pasi nzuri ya Said Ndemla akiwa peke yake na kupiga shuti pembeni kwa kipa Juma Kaseja.
Baada ya Simba kupata bao mashabiki wa Yanga walikaa kimya hali iliyomfanya mwenyekiti wao Yusuf Manji kusimama na kuwataka washangilie huku akionyesha vidole vitano. Jambo lililowafanya mashabiki wa Simba kuanza kuzomea kwa nguvu.
Tambwe alipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 43 baada ya Ramadhani Singano kuchezewa vibaya na David Luhende, kabla ya kuhitimisha kwa bao la tatu dakika ya 60, akitumia vizuri uzembe wa Kaseja kupachika bao la tatu.
Manji aliinuka kwenye kiti chake na kwenda kumkumbatia Zaccaria Hanspope na kuondoka uwanjani hali iliyowafanya mashabiki wa Simba kumzomea.
Okwi aliingia akitokea benchi na kuifungia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 79, akimalizia vizuri krosi ya Haruna Niyonzima.
Mashabiki wa Simba walikuwa wakiwakejeli wenzao wa Yanga kwa kuwaambia waendelee kusajili wachezaji wa Simba faida yake wameiona.
Baada ya kukabidhiwa kombe mashabiki wa Simba walizunguka nalo, na wengine wakisukuma gari la Hanspope huku wakiimba ‘Okwi, Okwi, Okwi..’
Katika mchezo huo Yanga walionekana kuwa na presha na kucheza zaidi kibinafsi kuliko kitimu kulinganisha na wapinzani wao Simba.
Yanga waliondoka kabisa mchezoni baada ya bao la Simba na kuwaacha viungo Mkude, Henry Joseph, Chombo wakifanya watakalo katika kuanzisha mashambulizi ya vijana hao wa Msimbazi.
Beki wa Yanga, Luhende alikuwa na bahati ya pekee kwa kukosa kupewa kadi nyekundu baada ya kumkwatua kwa nyuma winga Simba, Singano na kusababisha penalti iliyofungwa na Tambwe.

No comments:

Post a Comment