Dec 20, 2013

JE WAJUA KUWA “ROHO YA MANDELA IMESINDIKIZWA NA NG’OMBE WA KAFARA KWENDA KUZIMU?



Mswahili mwenzangu usishangae hili, Mambo ndivyo yalivyokuwa katika Mazishi ya aliyekuwa shujaa wa Afrika na Ulimwengu Hayati Nelson Mandela kuwa mazishi yake ya Kimila yaliambatana na shughuli za uchinjwaji wa ngombe dume (fahari) kisha damu ya ng’ombe huyo kumwagiwa juu ya kaburi lake

Kiongozi wa jamii ya Xhosa (lugha ya Waaba Thembu), Nokuzola Mndende alisema kuwa endapo serikali itapuuza matakwa yao ipo hatari ya Mandela kutopokelewa na miungu hivyo roho yake kurejea duniani na kuisumbua familia yake.

“Zitakuwa ni mila na desturi za jadi, serikali inapaswa kutupa nafasi na isituingilie. Ng’ombe dume (fahali) atachinjwa kwa ajili ya kumsindikiza marehemu kaburini,” alisema kiongozi huyo bila kupindisha maneno kinywani.

Aliongeza: “Katika utaratibu huu wa mazishi ya kimila ni familia ya Mandela pekee ndiyo watakaohusika kumwandalia safari njema Madiba.”

Kwa mujibu wa desturi za mazishi za kabila hilo, mtu aliyefariki dunia endapo alikuwa kiongozi, hupewa heshima ya kuchinjiwa ng’ombe dume ili amsindikize ambapo damu yake hunyunyiziwa juu ya kaburi.   

TARATIBU ZA MAZISHI ZA KIKABILA

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, zipo taratibu maalum ambazo ni lazima zifuatwe wakati wa mazishi ya mtu wa kabila moja na mzee Mandela.

Baada ya mtu kufariki dunia, ni jukumu la wanafamilia ya marehemu kutangaza msiba huo kwa ndugu na jamaa ili waweze kukutana na kusaidiana wakati wa mazishi.

Kabla ya ujio wa vyumba vya kisasa vya kuhifadhia maiti (mochwari), Waaba Thembu walikuwa wakimzika mtu siku hiyohiyo kwa kuhofia mwili wake kuharibika.

Kabla ya kufanyika kwa mazishi, taratibu zinasema vyombo vyote vilivyomo ndani ya nyumba hutolewa nje na wanawake wanaohusiana na marehemu ni lazima wafanye usafi katika nyumba aliyokuwa akiishi.

Katika siku za nyuma, kuta za kibanda kikubwa kilichokuwa kikitumiwa na marehemu kulala kilikandikwa udongo, lakini hivi sasa nyumba kubwa kwa kawaida husafishwa na kupakwa rangi upya.

Baada ya usafi huo, mkeka wa kiasili huwekwa katika chumba kikubwa cha kulala ambako mjane wa marehemu hutakiwa kukalia mkeka huo unaowekwa chini ya dirisha.

Uchaguzi wa ng’ombe mnono wa kiume hutegemea na umuhimu wa marehemu na wanaume ndiyo wanaopika nyama hiyo katika vyungu vya kikabila ikichemshwa bila kuwekwa kiungo chochote.

Tukio hili huitwa Umkhapho inayodaiwa kuwa  ni mizimu ya kumsindikiza mtu aliyefariki dunia.


No comments:

Post a Comment