SIKU chache baada ya Bodi ya
Filamu Tanzania (TFB) kuzuia filamu ya mkongwe katika sinema za Kibongo,
Mahsein Awadh Said ‘Dk. Cheni’ ijulikanayo kwa jina la Nimekubali isiingie
sokoni kwa madai kuwa imekiuka maadili ya Kitanzania, msanii huyo ameibuka na
kueleza kinagaubaga, Risasi
Jumamosi limenasa sauti yake. Akizungumza na
mwandishi wetu Jumatano ya wiki hii maeneo ya MlimaniCity
jijini Dar, msanii huyo alisema amesikitishwa na maamuzi ya bodi hiyo huku
akidai kuwa lengo la filamu hiyo ni kukemea tabia za kishoga zinazoendelea
kuibuka kwa vijana ikiwa ni pamoja na kupinga uhalali wa ndoa za jinsia moja.
Katika maelezo
hayo, DK. Cheni ambaye huzitendea haki filamu zake kwa kuvaa uhusika halisi,
alisema moja ya kigezo ambacho bodi hiyo imekitumia kuzuia filamu hiyo ni
pamoja na muonekano wa bango la filamu hiyo ambalo linamuonesha msanii huyo
akiwa amevaa vazi la shera huku akiwa amejiremba kwa madai kuwa ni kuchochea ushoga
jambo ambalo msanii huyo amelipinga vibaya. “Eti ushoga wangu
uko kwenye kujiremba sana, hakika wamenionea sana, lengo letu ni kuonya na kukemea vikali vitendo vya
ushoga na ndoa za jinsia moja, huwezi kuelimisha bila kuonesha madhara yake kwa
vitendo kama ilivyo ndani ya filamu hiyo.
Mkurugenzi wa bodi ya filamu, Joyce
Fissoo.
“Lakini, ndani ya
filamu hiyo, kuna kipande ambacho kinaonesha kiongozi wa serikali akikemea
kitendo hicho, sasa hapo ushoga wangu uko wapi? Kuvalia shera kwenye kava? Siyo
sahihi,” alisema Dk. Cheni.
Mbali na kava hilo,
msanii huyo alidai haoni kosa lolote katika filamu hiyo hivyo ataendelea
kupigania haki yake na kwamba hayuko tayari kuonewa. Jitihada za kumpa
mkurugenzi wa bodi ya filamu, Joyce Fissoo ili kuelezea juu ya sekeseke hilo, ziligonga mwamba
hadi gazeti hili linaingia mtamboni lakini imedaiwa kuwa bodi hiyo itasimamia
msimamo wake.
No comments:
Post a Comment